MBUNGE WA CHADEMA BAADA YA KUMPIGA MATEKE ASKARI WA BUNGE NA KUJIFICHA SASA AJISALIMISHA POLISI MWENYEWE!!

0


BAADA ya Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kumsaka
kwa siku mbili bila mafanikio mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu
(CHADEMA), akidaiwa kumpiga na kumjeruhi mmoja
wa askari wa Bunge, hatimaye alijisalimisha
mwenyewe jana jioni.
 
Taarifa zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni,
Sugu alikwenda polisi akiongozana na Mwenyekiti
wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na wabunge Tundu
Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na
Joshua Nassari (Arumeru Mashariki).
Akizungumza na mwandishi wetu, Mnyika alisema
kuwa Sugu hakukamatwa bali alijipeleka mwenyewe
polisi kwa hiari yake na kwamba jioni hiyo majira ya
saa 1:10 alikuwa akiandikisha maelezo yake.
 
Wakati Sugu akijisalimisha, wanasheria wa Bunge
nao walikuwa wamejifungia kuangalia namna ya
kumkabidhi mbunge huyo mikononi mwa sheria.
Juzi na jana viwanja vya Bunge vilitawaliwa na idadi
kubwa ya polisi waliotumwa kumkamata Sugu lakini
mpaka Bunge linaahirishwa jioni haikujulikana ni
wapi alikokuwa mbunge huyo.
Mbunge huyo juzi baada ya kubebwa mzobemzobe
na askari wa Bunge na kisha kutolewa nje ya ukumbi,
inadaiwa kuwa alimpiga ngumi mmoja wa askari
aliyemtuhumu kuwa alikuwa amempia ngumi wakati
wakimtoka nje.
 
Askari hao juzi jioni walikuwa kwenye vikundi
vikundi nje ya ukumbi wa Pius Msekwa ambako
kulikuwa kukifanyika mkutano wa wabunge wa
upinzani ambapo Sugu pia alikuwa miongoni mwao.
Kutokamatwa kwa Sugu kumewashangaza wengi
waliokuwa karibu na askari hao kwa kuwa alikuwa
amekaa jirani nao akizungumza na wenzake kabla ya
kuanza kwa kikao chao.
 
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa askari hao
walishindwa kumkamata Sugu kwa kuwa
hapakuwepo na amri ya kukamatwa kwake na hata
ilipotolewa alikuwa ameshaondoka katika viwanja
vya Bunge.
 
Mpaka Bunge linaahirishwa juzi jioni, idadi kubwa ya
askari walikuwa nje ya milango na korido zilipo ofisi
za kambi ya upinzani wakimsubiri Sugu bila
mafanikio.
 
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa miongoni mwa
mambo yaliyochangia askari kusuasua kukamatwa
kwa Sugu ni kutokana na kinga ya kibunge aliyonayo
na pia kosa analotuhumiwa kulifanya alilifanya akiwa
kwenye viwanja vya Bunge.
 
“Tulipata mtanziko wa kumkamata haraka haraka,
ilibidi lazima tuwasiliane na ofisi ya Spika kujua
taratibu za kumkamata kiongozi huyo hasa kwa kuwa
alifanya kosa hilo akiwa bungeni,” kilisema chanzo
kimoja.
 
Wakati askari wakihaha kumtafuta Sugu, mbunge wa
Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), jana
aliomba mwongozo wa Spika kuhusu tukio la vurugu
zilizotokea juzi bungeni hasa tukio la Sugu kumpiga
askari.
 
Sendeka alisema tukio hilo limelidhalilisha Bunge na
askari wanaowalinda, hivyo akataka liweke wazi ni
hatua gani zitakazochukuliwa dhidi ya mbunge huyo
ili kulinda heshima ya chombo hicho.
 
“Nataka nijue ibara ya 100 ambayo humpa kinga
mbunge na uhuru wa mawazo akiwa ndani ya Bunge
inatumikaje katika tukio hili?
“Je, Bunge litalindaje heshima yake dhidi ya tukio hili
lililofanywa na mbunge mwenzetu?” alihoji.
Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge,
Jenister Mhagama, alisema tukio hilo ni geni hivyo
Bunge limeshindwa kutoa jibu la mara moja.
 
“Jambo hili halijawahi kutokea katika historia ya
Bunge, sasa nami nitalifikisha kwa wanasheria wa
Bunge wanishauri namna ya kulishughulikia na
baada ya hapo nitatoa mwongozo,” alisema.
Akitoa mwongozo huo muda mfupi kabla ya Bunge
kuahirishwa jana jioni, Naibu Spika, Job Ndugai,
alisema kuwa bado wanashauriana na wanasheria
kuona kanuni zinawaelekezaje.
 
Alisema kuwa licha ya tukio hilo kutokea katika eneo
la Bunge bado kitendo hicho ni cha jinai na hivyo,
mtuhumiwa atashughulikiwa kisheria.
“Ni sawa na jaji yuko mahakamani ambapo kuna
kinga kama za Bunge halafu jaji mwenzake ampige
ngumi. Huyo lazima achukuliwe hatua hawezi
kuachwa. Kinga zetu ziko kwenye uhuru wa mawazo
tu,” alisema.
 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, juzi lilitangaza
kumsaka Sugu kwa tuhuma za kufanya vurugu na
kumjeruhi askari wa Bunge.
“Lakini tuna mashaka sana na hatua yake aliyoifanya
nje ya ukumbi ambapo alimvamia na kumpiga ngumi
nzito Koplo Nikwisa Nkisu ambaye alijeruhiwa jicho,”
alisema mmoja wa askari ambaye hakutaka jina lake
litajwe.
 
Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Dodoma ASP Jumanne
Kim, juzi jioni alithibitisha kusakwa kwa mbunge
huyo aliyeondoka maeneo ya Bunge mchana akiwa
ndani ya gari la kiongozi mkuu wa kambi rasmi ya
upinzani bungeni, Freeman Mbowe.

0 comments: